FAST JET SASA KUJIENDESHA, NI BAADA YA KUSITISHIWA UFADHILI

Dar es Salaam. Kampuni ya ndege ya Fastjet Plc ya Uingereza inapanga kusitisha ufadhili wake kwa Fastjet Tanzania.

Hali hiyo inatokana na mwenendo mbaya wa biashara uliosababisha ukata katika kampuni hiyo, lakini Fastjet Tanzania imewatoa wasiwasi wateja wake na kueleza kuwa itaendelea kutoa huduma kama kawaida.

Juzi, Fastjet Plc ilitoa taarifa ya mwenendo wake wa fedha kuwa inakabiliwa na upungufu mkubwa wa fedha kiasi cha kulazimika kuzitafuta kwa kufanya harambee na endapo hazitatosha basi itasitisha huduma zake nchini.

“Tunazungumza na wanahisa kufanya harambee kupata fedha ya ziada. Kwa hali ilivyo, Tunaweza tukasitisha huduma zetu nchini Tanzania,” ilisema menejimenti ya kampuni hiyo yenye makao yake Uingereza.

Kampuni hiyo ya usafiri nafuu wa anga imesema uamuzi wa kujitoa unatokana na changamoto za biashara zilizopo nchini hivyo majukumu yote ya uendeshaji na ugharamiaji yatabaki kwa bodi ya wakurugenzi wa Fastjet Tanzania.

Licha ya msimamo huo, mkurugenzi mkuu wa Fastjet Tanzania, Derrick Luembe alisema hawana mpango wa kusitisha huduma na wana fedha za kutosha kujiendesha.

“Fastjet Tanzania inaweza kujiendesha. Kuna fedha nyingi kampuni itakuwa nazo kwa kujiondoa kwake Fastjet Plc. Bado tuna vyanzo vingine vya mapato kukidhi mahitaji yetu na tunaendelea kuingia mikataba mipya na wateja wetu,” alisema Luembe.

Kwa sasa, ndege za shirika hilo zinaruka na kutua Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Kilimanjaro, Lusaka na Zimbabwe.

“Mwezi uliopita tumeboresha huduma baada ya kusikiliza maoni ya wateja wetu. Licha ya bei nafuu tunayotoza, mteja sasa anapata vitafutwa na vinywaji akiwa safarini.”

Related posts