Waziri wa mambo ya Nchi za Kigeni wa Ujerumani Heiko Maas amelitaka Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hatimaye kuanzisha mazungumzo muhimu kuhusu mageuzi katika Baraza la Usalama la umoja huo

 

Maas amesema Baraza hilo halijabdilika tangu lilipoasisiwa mwaka wa 1945, licha ya kuongezeka mara tatu kwa idadi ya watu duniani tangu wakati huo, na kuongezeka mara nne idadi ya nchi wanachama katika kipindi hicho.

Ujerumani kwa muda mrefu imekuwa ikishinikiza megeuzi ya Umoja wa Mataifa na lengo kuu la kutaka kiti cha kudumu katika Baraza la Usalama. China, Ufaransa, Urusi, Uingereza na Marekani ni wanachama wa kudumu wakiwa na kura za turufu kuhusu maamuzi ya Baraza hilo.

Ujerumani imechaguliwa kuwa mmoja wa wanachama 10 wasio wa kudumu kwa muhula mmoja wa miaka miwili kuanzia Januari 2019.

Maas amesema wakati wa hotuba yake kwa baraza hilo kuwa ni aibu kwamba shirika la Umoja wa Mataifa la kuwashughulikia Wakimbizi UNHCR linapungukiwa na fedha za kuwasaidia mamilioni ya Wasyria ambao wamekimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo. Ameyataka mataifa mengine tajiri kutoa mchango.


Related posts