MSICHANA ATISHIA KUJIUA ENDAPO ATALAZIMISHWA KUENDELEA NA MASOMO

Mwanafunzi mmoja wa kike (15) wa kidato cha kwanza amenusurika kufa kwa kujinyonga baada ya kukerwa na wazazi wake wanaomlazimisha aendelee na masomo.

Msichana huyo wa shule ya Sekondari Nsemlwa, Manispaa ya Mpanda, mkoani Katavi amefikia uamuzi huo ili asisumbuliwe na wazazi wake wakati yeye hataki kusoma.

Siku ya tukio msichana huyo anadaiwa kuandaa kitanzi na stuli ili atekeleze mpango huo kabla ya kuokolewa na baba yake mzazi Bushiri Joseph ambaye alimkuta tayari amepanda kwenye kiti hicho.

Mwanafunzi huyo pamoja  mwenzake wa kiume mwenye umri wa miaka 16, anayesoma kidato cha pili katika shule hiyo, wanadaiwa kuwa watoro sugu na kutishia kujiua kwa kujinyonga kwa kamba au kunywa sumu iwapo wazazi na walimu wao wataendelea kuwalazimisha kuendelea na masomo.

Licha ya kuhojiwa na wazazi na walimu wao, wanafunzi hao hawakuwa tayari kueleza kinachowasababisha wakatae kuendelea na masomo na badala yake wamekuwa wakitishia kujiua kama watalazimishwa kurejea shuleni.

Inadaiwa kuwa wazazi wa wanafunzi hao wameshawafikisha kituo cha polisi bila mafanikio, wakiwa na msimamo wao wa kujiua.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Edgar Mwaisunga, aliwaambia waandishi wa habari kuwa mwanafunzi huyo alifikishwa na baba yake mzazi shuleni hapo kujiunga na kidato cha kwanza Januari, mwaka huu.

Facebook Comments

Related posts