QUEEN LATIFAH: “Vijana, Huu Sio Mwisho Wa Dunia. Hii Ni Dunia Yenu”

UKIACHILIA mbali uwezo wake mkubwa wa uandishi wa mashairi “Konki” katika muziki wa Hip Hop, Ufundi wake “Mtamu” kwenye suala zima la “Ku-flow” kunako Kazi zake na hata zile ambazo anashirikishwa, Mkongwe kwenye utamaduni wa “hip Hop” Duniani kwa upande wa Jinsia ya Kike, Queen Latifah pia ni miongoni mwa Waigizaji Bora sana katika ulimwengu wa filamu Duniani na kila mtu analiheshimu hilo kwa nafasi yake.

Lakini nje ya Vipaji hivyo alivyonavyo, Queen Latifah pia ni miongoni mwa Wasanii ambao waliamua kusimama katika upande wa Harakati za kimaendeleo hasa kwa jamii mbali mbali na hata vijana, ili kuhakikisha wanapata uelewa na elimu kupititia uzoefu ambao wamekwishaupata tayari tangu enzi hizo wanaingia katika Tasnia ya Burudani.

Kutokana na Vugu vugu la maandamano ambayo yanaendelea duniani dhidi ya Ubaguzi wa Rangi, Queen Latifah amtoa Ushauri kwa vijana wote duniani ambao wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha vitendo vya kikatili na unyanyasaji wa viongozi na askari polisi vinakomeshwa duniani, kuhakikisha kuwa wanakuwa mstari wa mbele kuwaondoa madarakani viongozi ambao hawasimamii misingi bora ya uongozi kwa raia wao.

Queen Latifah (50) amefafanua kwa undani kuwa, Vijana wote duniania, hawatakiwi kuchukulia matukio haya yanayoendelea maeneo mbali mbali kama ndio mwisho wa dunia, bali wao ndio nguzo kubwa ya dunia mpya ijayo kwa sababu wanatakiwa kusimama na kuhakikisha wanaondoa changamoto hizi ambazo zimekuwepo tangu zamani.

QUEEN LATIFAH: Anaamini kuwa Vijana ndio watasimama mbele, na wao kama wazoefu wa matukio haya, watasimama nyuma yao kuwaongezea ujuzi, elimu na namna ambavyo watashirkiana kutokomeza matukio haya ya kibaguzi ambayo hayajaanzia kwao tu. (Picha :Queen Latifah Instagram)

Pia Queen Latifah ambaye jina lake halisi ni Dana Elaine Owens, amesisitiza kuwa wao hivi sasa umri umesogea kwa asilimia fulani, na vijana ndio wanaotakiwa kuhakikisha wanapambana juu chini ili kuijenga Dunia mpya kwa kushirikiana kwa ukaribu, kuondoa utengano, kuacha ubinafsi, na hata kupiga Kura kinapofika kipindi cha uchaguzi ili kuweka viongozi sahihi, na kuondoa viongozi wasio sahihi ambao wamekuwa ni chachu ya matukio mbaya ya aina hiyo ambayo yamekuwa yakikumbatiwa tangu enzi za mababu zetu na hata wazazi wetu.

” Hili Pia litapita, hivyo msifikirie huu ndio mwisho wa Dunia. Chukulieni hili kama mwanzo wenu, na chukulieni hii nafasi kama mwanya wa kuikomboa dunia yenu. Hii ni Dunia Yenu. Jumuikeni katika Michakato chanya. Kama ni Kupiga Kura pigeni kura kuwaondoa wasiofaa na kuwaweka madarakani wanaofaa. Lakini pia, endeleeni kujumuika pamoja. Tengenezeni mitandao chanya, endeleeni kuja na mawazo na mbinu mpya. Shirikishaneni na acheni ubinafsi” alisistiza Queen Latifah

Related posts