Maelfu waandamana katika mji mkuu Belarus licha ya ukandamizaji

Maelfu ya wafuasi wa upinzani waliandamana jana mjini Minsk wakidai kumalizika kwa utawala wa kiongozi wa kiimla wa Belarus Alexander Lukashenko wakati kukiwa na ulinzi mkali na licha ya watu kadhaa kukamatwa. Maandamano ya Belarus yameingia wiki ya tatu tangu kufanyika uchaguzi wa rais wa Agosti 9 ambao Lukashenko alidai ushindi. Kiongozi wa upinzani Svetlana Thikanovskaya anasema yeye ndiye aliyekuwa mshindi wa kweli. Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 100,000 walihudhuria maandamano ya jana ambao yameelezwa kuwa makubwa kuwahi kushudiwa nchini humo tangu ilipopata uhuru kutoka kwa uliokuwa muungano wa Kisovieti. Yalikuja katika siku ambayo Lukashenko aliadhimisha miaka 66 ya kuzaliwa kwake. Umati ulikusanyika nje ya makaazi rasmi ya rais huyo, Kasri la Uhuru, ambalo lililindwa na polisi wa kuzima ghasia na vikosi maalum vikisaidiwa na walenga shabaha waliokuwa kwenye mapaa.

Related posts