Mgombea urais wa Shirikisho la Riadha Tanzania, Nsolo Malongo Mlozi, amesema kuwa endapo atachaguliwa kushika wadhifa huo, atahakikisha anasimamia ipasavyo katiba ya shirikisho hilo.
Akizungumza na vyombo vya habari, Nsolo alisema vipaumbele vyake vitahusisha kulifanya shirikisho kuwa ngazi muhimu ya kukuza vipaji na kupata wanariadha bora watakaoliwakilisha Taifa kwenye mashindano ya Kitaifa na Kimataifa.
Amesema kuwa atatumia elimu yake, uwezo alionao na uzoefu wa zaidi ya miaka nane alioupata katika kufanya kazi zake za riadha ili kuhakikisha shirikisho hilo linazalisha wanariadha bora.
Nsolo alibainisha kuwa endapo atachaguliwa atadumisha ushirikiano na wadau wa mchezo huo katika ngazi zote kuanzia wilaya, Mikoa hadi taifa na atapitia katiba ili kuifanyia marekebisho yatakayoongeza ufanisi zaidi.
Aidha ameongeza mipango yake ni kushirikiana na wadau wa mchezo huo, ikiwemo serikali ili kuliwezesha shirikisho hilo kutekeleza majukumu yake bila kukwama .
Uchaguzi wa Shirikisho la Riadha Tanzania unatarajiwa kufanyika Jumamosi, tarehe 16 Agosti 2025, mkoani Mwanza katika hoteli ya Aden Palace