Madagascar yatangaza amri ya kutotoka nje usiku kufuatia maandamano makali

Serikali ya Madagascar, kisiwa kilicho katika Bahari ya Hindi, siku ya Alhamisi kimetangaza marufuku ya kutotoka nje usiku kufuatia maandamano makali. Polisi walitumia risasi za mpira na mabomu ya machozi kuzima maandamano dhidi ya kuendelea kukatika kwa maji na umeme.

Mamia ya waandamanaji walijitokeza barabarani kuelezea hasira zao kutokana na kuendelea kukatika kwa umeme , ambapo mara nyingi nyumba na biashara hukaa bila umeme kwa zaidi ya saa 12.

Waandamanaji walifunga barabara kwa matairi ya moto na mawe. Siku ya Alhamisi alasiri, uporaji uliripotiwa katika biashara kadhaa, maduka ya vifaa na benki katika mji mkuu.

Vituo kadhaa vya mafuta nchini pia vilichomwa moto.

Vyombo vya habari vya ndani viliripoti siku ya Alhamisi kwamba nyumba tatu za wanasiasa walio karibu na Rais Nirina Rajoelina pia zilishambuliwa na waandamanaji.

Mkuu wa polisi Angelo Ravelonarivo ametangaza kwamba marufuku kali ya kutotoka nje usiku itawekwa kuanzia saa 1:00 jioni Alhamisi hadi 11 alfajiri Ijumaa hadi utulivu urejee. Kulingana na Ravelonarivo, uamuzi huu ulifanywa ili kulinda vyema raia.

“Maji na umeme ni mahitaji ya kimsingi ya binadamu,” “Tuseme,” “Wana Madagascar amkeni” ni baadhi ya jumbe zilizokuwa zikionyeshwa kwenye mabango hayo.

Baadhi yao walibeba bendera nyeusi zenye nembo ya Fuvu la One Piece —nembo ya maandamano ya kupinga utawala nchini Nepal katika wiki za hivi karibuni—wakati huu wakiwa wamevalia kofia ya kitamaduni ya Kimadagascar.

Idadi kamili ya majeruhi na vifo wakati wa maandamano haijajulikana.

Vuguvugu la maandamano, linaloongozwa hasa na vijana, lilianza kushika kasi siku chache zilizopita kwenye mitandao ya kijamii, hasa Facebook.

Katika majimbo ya nchi hiyo machafuko pia yaliripotiwa katika afisi za shirika la taifa la maji na umeme jambo ambalo waandamanaji wanaamini kuwa ndio chanzo cha matatizo ya nchi hiyo.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii