Watu wawili wafariki ajali ya basi na lori Geita

Watu wawili wamefariki dunia katika ajali iliyohusisha basi la abiria la Kampuni ya Mallesa na gari la mizigo iliyotokea katika kijiji cha Rumasa, kata ya Butengorumasa, tarafa ya Buseresere, wilayani Chato mkoani Geita.

Akizungumza kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema jeshi la polisi linaendelea kufanya uchunguzi zaidi kubaini chanzo chake.

Kwa mujibu wa maelezo ya awali, basi hilo la Mallesa lilikuwa likitokea mkoani Dar es Salaam kuelekea Geita, wakati gari la mizigo lililokuwa limebeba vifaa vya ujenzi lilikuwa likitokea mkoani Mwanza kwenda wilayani Kibondo, mkoani Kigoma.

Ajali hiyo imetokea majira ya saa saba usiku na chanzo chake bado hakijajulikana mara moja.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii