Wanajeshi 15 wa Pakistan wameuawa katika mapigano makali kati ya vikosi vya Taliban na jeshi la Pakistan karibu na mpaka wa Durand, baada ya mashambulizi ya anga yaliyotekelezwa na Pakistan ndani ya ardhi ya Afghanistan, ikiwemo mji mkuu, Kabul.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na msemaji wa serikali ya mkoa wa Helmand, Mawlawi Mohammad Qasim Riaz, vikosi vya Taliban vilitekeleza operesheni ya kijeshi usiku uliopita katika wilaya ya Bahrampur, mkoani Helmand, kama jibu kwa mashambulizi ya Pakistan. Katika operesheni hiyo, alisema kuwa wanajeshi 15 wa Pakistan waliuawa.
Aidha, Riaz alifafanua kuwa vikosi vya Afghanistan vilifanikiwa kuteka vituo vitatu vya kijeshi vya Pakistan vilivyokuwa katika eneo hilo la mpakani. Silaha na risasi zilizokuwemo katika vituo hivyo pia zilinaswa na kuingizwa mikononi mwa majeshi ya Afghanistan.
Mapigano haya yanajiri katika kipindi cha mvutano unaoendelea kati ya mataifa hayo mawili, huku Pakistan ikituhumu Afghanistan kwa kuwapa hifadhi wapiganaji wa kundi la Tehrik-i-Taliban Pakistan (TTP), wakati Taliban wakikanusha na kuelekeza lawama kwa Pakistan kwa uvamizi wa mara kwa mara wa anga ndani ya mipaka ya Afghanistan.