Kikosi kilirejea jana Dar es Salaam, leo vijana wamepumzika na kesho watarudi Mo Simba Arena kuanza maandalizi ya mchezo wa Jumapili.
Tunayo furaha ya kocha wetu Seleman Matola amemaliza adhabu yake hivyo atakuwepo kwenye benchi Jumapili kuendelea na majukumu yake na mchezaji wetu Alassane Kanté atarudi uwanjani kuendelea kuitumikia Simba.”
“Kuelekea mchezo huu tumeweka viingilio vya kitajiri. Viingilio ni Tanzanite - Tsh. 250,000, Platinum - Tsh. 150,000, VIP A - Tsh. 30,000, VIP B - Tsh. 20,000, VIP C - Tsh. 10,000 na Mzunguko - Tsh. 5,000.”
“Afrika hii timu zenye uhakika wa kucheza makundi mara saba mfululizo ni Al Ahly na Mamelodi na sisi tunaongezeka hapo. Ni mechi ambayo inatuongezea thamani kwenye klabu yetu.
Na Mwanasimba asitokee akaidharau hii mechi, tuutizame huu mchezo kama mchezo mpya.
Itakuwa haina maana yoyote tuje hapa tufungwe bao moja au mbili au twende matuta hatupo tayari kuona hiyo fedheha. Tuhesabu bado ni bilabila.”
“Mpaka sasa sisi tumeshinda mechi moja na bado hatujafuzu. Mechi hii ya kufuzu tunataka kujaza uwanja wa Mkapa, hatutakiwi kuchukulia poa, kwenye mpira hakuna kitu cha kawaida.
Twendeni tukaujaze Uwanja wa Benjamini Mkapa. Na sare yetu siku ya Jumapili itakuwa ni jezi nyekundu ya kuscan. Usije na jezi ya zamani tafadhali, kila Mwanasimba aje na jezi mpya ya Jayrutty.”
“Wanasimba tunasababu za kuja uwanjani maana mechi iliyopita tuliangalizia mchezo tukiwa Coco Beach, ilituuma. Tunalazimika kwenda uwanjani ili kumkaribisha Meneja Dimitar Pantev akutane na Wanasimba kwa mara ya kwanza, aione Simba Sports Club ipoje. Kwa kifupi Oktoba 26 itakuwa Simba Day ya Pantev maana ile nyingine hakuwepo.”- Semaji Ahmed Ally.
Ikumbukwe kuwa mpaka sasa simba wapo makao mkuu ya TFF kwa lengo la kuzungumzia mchezo wa marudiano dhidi ya Nsingizini Hotspurs Sababu ya kufanyia hapa TFF ni kuonyesha heshima yetu kwa mamlaka hii na mafanikio ambayo yamepatikana chini ya uongozi wa Wallace Karia.”
“Mchezo wa marudiano dhidi ya Nsingizini Hotspurs itachezwa Jumapili Oktoba 26 mwaka huu kuanzia saa 10:00 jioni. Nitumie nafasi hii kuwatangazia mashabiki wetu kwamba mchezo huu wataruhusiwa kuingia uwanjani. Tunawashukuru mashabiki wote ambao walijitoa kwa hali na mali kulipia faini, matoleo hayakuwa makubwa sana lakini hicho tulichopata klabu tutaongezea.”
“Uongozi wa Simba tunakemea vitendo vyote ambavyo vitasababisha kufungiwa. Kuelekea mchezo huu ni marufuku kuwasha moto na ni marufuku shabiki kuingia uwanjani eneo la pitch. Haya ndio mambo mawili ambayo yametuingiza kwenye adhabu.”
“Wapo watu wanavaa jezi ya Simba lakini sio mashabiki wa Simba, wananunua tiketi na kuja uwnajani ili kuja kutuharibia. Tunawatangazia yeyote ambaye atafanya vitendo hivi kwa makusudi tunamtangazia mtu huyu tutaruka nae mazima hapo hapo uwanjani.”- Semaji Ahmed Ally.