KIONGOZI wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka amejitetea dhidi ya shutumu kuwa hajatekeleza miradi ya maendeleo kwa miaka 40 aliyodumu uongozini akifichua kuwa alikataa shinikizo za kuweka lami katika barabara ya kuelekea kwake Tseikuru.
Wiki jana kulikuwa na majibizano makali kati ya Rais William Ruto na Bw Musyoka kuhusu barabara zinazopatikana katika Kaunti ya Kitui huku akisema Bw Musyoka licha ya kuwa serikalini kwa miaka 40 hakujenga barabara ya kuelekea kwake nyumbani Tseikuru, Mwingi Kaskazini.
Rais alishangaa ni vipi Bw Musyoka ataendeleza Kenya kama si mchapakazi kwa miaka mingi aliyokuwa uongozini.
Bw Musyoka alisema yeye si kiongozi mwenye tamaa wala hajutii kuwa alianzisha miradi mingi bila kupendelea kwake.
“Ningependa niambie Rais Ruto na wandani wake kwamba kuna usemi kwamba watoto wanakula kwanza, watu wazima wale wa mwisho na ninaamini kwamba mwishowe barabara ya lami itafika nyumbani Tseikuru.”
Alifichua kuwa alipokuwa makamu wa rais, Katibu wa Wizara ya Barabara wa wakati huo, Mhandisi Michael Kamau alitaka kuweka lami ya kilomita 21 katika barabara ya Tseikuru-Kyuso lakini akakataa na kusema ianzishwe kutoka Mwingi hadi Kamuongo.
“Lazima viongozi waonyeshe haki wala si ubinafsi. Nilikataa barabara hiyo kwa sababu mimi si mtu mbinafsi. Nilionelea barabara ya Mwingi-Kyuso-Garissa itengenezwe kwanza,” akasema.
Bw Musyoka alitaja mradi wa maji kutoka Kiambere hadi mji wa Mwingi ambao umewasaidia wakazi wengi wa eneo hilo kama matunda ya jitihada zake.
By Musyoka alisema kuwa Rais Ruto sasa anamlenga baada ya kubaini kuwa yeye ndiye kiongozi bora zaidi katika upinzani anayeweza kumbwaga uchaguzini 2027.
Alidai Rais amekuwa akijipendelea kwa kuelekeza miradi katika makazi yake.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime