Serikali imepiga hatua kubwa katika kulinda afya na ustawi wa wazee baada ya kufanikiwa kutoa vitambulisho vya matibabu ya bure pamoja na bima za afya kwa wazee zaidi ya 1,256,544 kote nchini.
Hatua hiyo imelenga kuhakikisha kundi hilo muhimu linapata huduma za afya bila vikwazo vya kifedha.
Aidha, serikali inaendelea kutoa huduma za matunzo katika makazi 13 ya wazee yanayomilikiwa na kusimamiwa na serikali, hatua inayolenga kuwapatia mazingira salama na yenye staha wazee wasiokuwa na msaada wa kifamilia.
Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk. Dorothy Gwajima, alisema kuwa katika kipindi cha mwaka 2022 hadi 2025, wizara hiyo imeendelea kutoa huduma za msingi kwa wazee ikiwemo chakula, malazi, mavazi pamoja na huduma za matibabu.
Dk. Gwajima alibainisha kuwa utekelezaji wa huduma hizo umefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupitia ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi, jambo lililochangia kuboresha maisha na hadhi ya wazee nchini.
Serikali imeahidi kuendelea kuboresha mifumo ya hifadhi ya jamii ili kuhakikisha wazee wanaishi maisha yenye heshima, afya njema na usalama.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime