Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) yameanza vibaya kwa mataifa ya Afrika Mashariki, Tanzania na Uganda, baada ya timu hizo kukubali kichapo katika mechi zao za ufunguzi zilizochezwa jana.
Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, ilishindwa kuhimili makali ya Nigeria baada ya kupoteza kwa mabao 2-1 katika mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa, licha ya kuonesha jitihada za kusaka matokeo chanya.
Kwa upande wa Uganda, hali ilikuwa ngumu zaidi kwa The Cranes baada ya kubamizwa kwa mabao 3-1 na Tunisia katika mechi iliyochezwa mjini Rabat, matokeo yaliyowaacha mashabiki wao wakiwa na wasiwasi kuhusu mustakabali wa timu hiyo kwenye michuano hiyo.
Hata hivyo, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) imewapa matumaini ya awali mashabiki wa soka wa Afrika Mashariki na Kati, baada ya kuibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Benin katika mechi yao ya kwanza ya kundi.
Katika michezo mingine, mabingwa wa Afrika Magharibi, Senegal maarufu kama Simba wa Teranga, walionesha ubora wao kwa kuicharaza Botswana kwa mabao 3-0, na kuanza vyema kampeni yao ya kutetea heshima ya bara hilo.
Michuano ya ufunguzi wa hatua ya makundi itaendelea leo kwa michezo minne, ikiwemo pambano linalosubiriwa kati ya Ivory Coast na Msumbiji, huku Algeria ikitarajiwa kuvaana na Sudan.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime