KLABU ya Simba imepiga hodi Mamelodi Sundowns nchini Afrika Kusini ikisema inahitaji kumsajili moja kwa moja beki wa kati anayeichezea timu hiyo kwa mkopo Rushine De Reuck baada ya kuridishwa na huduma yake.
Simba ilimchukua beki hiyo kwa mkopo wa mwaka mmoja ikiwa na kipengele cha kumnunua moja kwa moja kama itaridishwa naye.
Habari kutoka ndani ya Simba zinasema mabosi wanataka kukamilisha dili hilo katika dirisha dogo la usajili wakihofia baadhi ya timu ‘kutia’ mguu kutaka kumsajili kwa dau kubwa kitu ambacho kitawapa ugumu hapo baadaye.
"Tunataka tukamilishe usajili huu haraka sana kipindi hiki cha dirisha dogo, uwezo wake tayari umeanza kuzishawishi baada ya klabu kuwasiliana na Mamelodi Sundowns, bahati nzuri katika mkataba wetu wa mkopo tumeweka kipengele cha sisi kwanza tuulizwe, kama hatutaki au tumeshindwa ndiyo auzwe kwingine," kilisema chanzo chetu.
Chanzo hicho kiliongeza hata hivyo mpaka kufikia jana, hakuna majibu yaliyotolewa na Mamelodi Sundowns kuhusiana na ofa ambayo Wekundu wa Msimbazi wameiwasilisha cha vigogo hao wa bondeni.
Taarifa zaidi zimesema Simba ilipeleka barua nyingine kwa Mamelodi Sundowns, mbali na Rushine, ambaye ana mabao mawili mpaka sasa kwenye Ligi Kuu, nyingine ni kumwomba tena mchezaji mwingine wa timu hiyo, Fawaaz Basadien, mwenye uwezo wa kucheza beki wa kushoto na kati.
"Kama nilivyowahi kukwambia huko nyuma, beki huyu naye tunamtaka kwa mkopo kipindi cha dirisha dogo, akituridhisha mwisho wa msimu naye tunaomba kumsajili wa moja kwa moja," aliongeza mtoa taarifa wetu.
Meneja Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, aliliambia gazeti hili kipindi cha dirisha dogo kutakuwa na maboresho ya kikosi, akiahidi pia hakuna mchezaji yoyote ambaye timu hiyo inamtaka anaweza kuondoka.