STRAIKA wa JKT Tanzania, Peter Paul, ambaye alienguliwa katika kikosi cha Timu ya Taifa (Taifa Stars), kilichoelekea Misri kuweka kambi ili kujiandaa na Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025), anaongoza kwa kufunga mabao ya vichwa kwenye Ligi Kuu Bara mpaka sasa.
Mchezaji huyo ambaye pia anaongoza katika orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu Tanzania Bara, akiwa amepachika mabao matano, anaonekana pia ni hatari kwa mipira ya vichwa.
Kwa mujibu wa takwimu za michezo za Nipashe, Peter, amepachika mabao matatu kwa kichwa mpaka sasa huku kukiwa hakuna mchezaji yoyote aliyefunga idadi hiyo ya magoli.
Kati ya mabao matano aliyofunga na kumfanya aongoze, straika huyo aliyesajiliwa msimu uliopita akitokea Dodoma, Jiji, matatu ameyafunga kwa njia hiyo.
Peter alikuwa katika kikosi cha awali cha Stars kilichokuwa na wachezaji 53, lakini alikuwa mmoja wa walioenguliwa kabla ya kubakia nyota 28 ambao kwa sasa wako Misri wakiendelea na maandalizi.
Takwimu zinaonyesha jumla ya mabao 17, yamefungwa kwa vichwa kwenye Ligi Kuu mpaka sasa.
Mchezaji anayefuatia kwa kufunga mabao mengi ya vichwa ni Matheo Antony wa Mbeya City akifanya hivyo mara mbili.
Wengine ambao majina yao ya klabu yapo kwenye mabano ni Rushine De Reuck, Chamou Karaboue na Wilson Nangu (Simba), Lassane Koume na Mudathir Yahaya (Yanga), Nassor Saadun na Feisal Salum (Azam), Oscar Mwajanga (Prisons), Haroub Mohamed (Coastal), Andrew Simchimba (Mtibwa), Mudrick Shehe (Fountain Gate) na Jaffar Kibaya wa Mashujaa FC.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime