Kiongozi wa zamani wa waasi nchini DRC Roger Lumbala amepatikana na hatia ya kushiriki katika uhalifu dhidi ya binadamu siku ya Jumatatu, Desemba 15.
Mwanasiasa huyo wa Kongo, aliyeshtakiwa kwa uhalifu uliofanywa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mwanzoni mwa miaka ya 2000, amehukumiwa kifungo cha miaka thelathini jela. Vyama vya kiraia vimekaribisha uamuzi huo kama wa kihistoria. Roger Lumbala na wakili wake aliyeteuliwa na mahakama, Bw. Vigier, wamekuwepo katika chumba cha mahakama kwa mara ya kwanza katika kikao hiki cha mwisho kwa kesi hiyo.
Ilikuwa saa 11:00 jioni wakati majaji walipoingia katika chumba cha mahakama katika mahakama ya Paris. Jaji mkuu aliomba kikao kukatishwa ili kumuuliza Roger Lumbala kama angependa kuhudhuria kikao kicho. Dakika chache baadaye, mshtakiwa aliingia, akiwa amezungukwa na maafisa wawili wa polisi. Mwanasheria wake aliyeteuliwa na mahakama, Wakili Vigier, ambaye hakuwa amehudhuria kesi hiyo wakati wa wiki tano, aliketi kwenye benchi la utetezi na kuzungumza naye maneno machache.
Kisha, jaji mkuu, akimhutubia Roger Lumbala moja kwa moja, alianza kusoma hukumu: "Bw. Lumbala," alisema, "mahakama imeamua: inakupata wewe na hatia ya kushiriki uhalifu dhidi ya ubinadamu kwa kila shtaka." Kisha jaji alitaja waathiriwa wasiopungua 30 na kukubali hatia ya Roger Lumbala, kupitia msaada na kuunga mkono, ubakaji, mateso, utumwa, utumwa wa kingono, kazi ya kulazimishwa, pamoja na wizi na uporaji. Hukumu hiyo ilitolewa: mbabe wa zamani wa vita aliyegeuka kuwa mwanasiasa alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na kupigwa marufuku kabisa kuikaa nchini Ufaransa.
Roger Lumbala alibaki amesimama, kimya, akisikiliza. Hakuna hata mmoja wa majaji aliyemtazama. Ana siku kumi za kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.
Majibu kutoka kwa waathiriwa yalikuwa ya haraka. "Kwa kweli ni hisia ya furaha na, kwangu mimi, pia uponyaji wa kisaikolojia," mmoja wao alisema baada ya uamuzi huo. "Baba yangu alipigwa risasi kama mnyama [na wapiganaji wa Roger Lumbala]. Tangu wakati huo, nimekuwa nikijiuliza kila mara ikiwa watu waliofanya hivi ni wanadamu kama sisi, lakini sasa najua kwamba hakuna 'watu wa ajabu' na kwamba kila mtu anawajibika mbele ya sheria. Hii inatuma ujumbe mzito kwa viongozi wengine wa kivita ambao wanaendelea kufanya vitisho nchini mwetu," aliongeza.
"Hukumu kama hii, kuhusu matukio yaliyotokea miaka 23 iliyopita, ni chanzo kikubwa cha kuridhika," alisema mwathiriwa mwingine, akikumbusha, "Wakati huo, [kundi la Roger Lumbala] liliniibia kila kitu nilichokuwa nacho na kujeruhi mkono wangu wa kulia. Baada ya hapo, walimchukua mjomba wangu ili auawe."
"Kujumuishwa kwa ubakaji kama uhalifu dhidi ya ubinadamu katika hukumu, majadiliano yaliyofanyika mbele ya [Roger Lumbala], na kushtakiwa kwake kwa uhalifu huu kama mshirika kunawakilisha ushindi mkubwa dhidi ya kutokujali. Pia ni ushindi mkubwa kwa waathiriwa ambao, miaka 22 baada ya matukio hayo, walikuwa na ujasiri wa kutoa ushahidi na kujitokeza mahakamani," alisema Wakili Bectarte, mwanasheria wa vyama vya kiraia.
"Hatua ya Mabadiliko"
Hukumu ya kifungo cha miaka 30 jela iliyotolewa kwa Roger Lumbala huko Paris ni "ya kihistoria" na "inaashiria mabadiliko," yalitangaza mashirika manane yasiyo ya kiserikali yanayofanya kazi kama vyama vya kiraia katika kesi hiyo. "Hukumu hii inatuma ujumbe mzito sana, ikionyesha kwamba wakati, wala umbali, wala nafasi za madaraka haziwezi kuwalinda wahusika au washirika wa uhalifu mkubwa," alisema Daniele Perissi, mratibu wa TRIAL International nchini DRC.
Lakini mashirika ya haki za binadamu ya Kongo na kimataifa pia yanajua kwamba mapambano haya yanabaki kuwa dhaifu. Wanaeleza kwamba hukumu katika kesi ya Lumbala inakuja "wakati ambapo vurugu" zinaendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, "licha ya makubaliano ya hivi karibuni ya Washington" kati ya pande zinazopigana.
Vita ambavyo vimeikumba mashariki mwa DRC kwa miaka 30, vikihusisha nchi jirani kama Rwanda na Uganda na kuendeshwa hasa na udhibiti wa madini na maliasili, vimegharimu maisha ya mamilioni ya watu na kusababisha wengi kuyahama makazi yao.
Ijapokuwa wababe watatu wa kivita—Thomas Lubanga, Germain Katanga, na Bosco Ntaganda—walihukumiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kati ya mwaka 2012 na 2021, mashirika yasiyo ya kiserikali yanasema kwamba hakuna mahakama ya kitaifa ya nchi yoyote inayodai mamlaka ya ulimwengu ambayo hapo awali ilitoa hukumu ya ukatili uliofanywa mashariki mwa DRC.