Waziri wa mambo ya nje wa Israel Gideon Saar ameahidi kwamba nchi yake itakuza uhusiano wenye mafanikio na Somaliland baada ya kuwa nchi ya kwanza kutambua uhuru wa eneo hilo lililojitenga na Somalia.
Katika ziara yake ya kwanza rasmi Somaliland, Saar amesema Israel itafungua ubalozi hivi karibuni mjini Hargeisa na kumteua balozi atakayewakilisha nchi hiyo ndani ya ardhi ya Somaliland, licha ya ukosoaji mkubwa wa kimataifa kuhusu uamuzi wake wa kulitambua eneo hilo, ambalo sehemu kubwa ya dunia inalichukulia kuwa sehemu ya Somalia.
Kwa mujibu wa nakala ya hotuba iliyoonekana na shirika la habari la AP, mwanadiplomasia huyo amesisitiza kuwa hakuna taifa litakaloielekeza Israel kuhusu nani wa kumtambua au nchi gani idumishe nayo uhusiano wa kidiplomasia.
Saar amesema uamuzi huo ni sehemu ya sera huru za Israel katika kutafuta ushirikiano wa kimkakati duniani.
Rais wa Somaliland Abdirahman Mohamed Abdullahi ameeleza kuwa ziara ya Saar "ina umuhimu wa kihistoria na kuashiria mwanzo wa enzi mpya ya ushirikiano" kati ya nchi hizo mbili.