TRUMP AAGIZA MAREKANI KUJIONDOA KATIKA MASHIRIKA 66 YA KIMATAIFA

Rais wa Marekani Donald Trump ameagiza nchi yake kujiondoa katika mashirika 66 ya kimataifa akieleza kuwa taasisi hizo hazihudumii tena maslahi ya taifa la Marekani.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu ya White House uamuzi huo umeainishwa katika hati ya maelekezo aliyosaini jana Jumatano huku ikielezwa kuwa hatua hiyo inaendana na sera ya “America First”, inayolenga kuweka mbele maslahi ya ndani ya Marekani.

Ikulu imesema kati ya mashirika hayo 31 ni ya Umoja wa Mataifa (UN) huku 35 mengine yakiwa ni taasisi zisizo za UN. Mashirika mengi yaliyoathiriwa yanahusiana na masuala ya mabadiliko ya tabianchi utawala wa kimataifa, ajira na maendeleo.

Utawala wa Trump umefafanua kuwa maeneo hayo yanachochea ajenda wanayoitaja kama “woke”, ambayo kwa mtazamo wao, haiendani na vipaumbele vya taifa la Marekani.

Miongoni mwa taasisi za UN zilizoathiriwa ni tume za kiuchumi na kijamii za Afrika, Asia-Pasifiki, Amerika ya Kusini na Karibiani pamoja na mashirika kama UN Trade and Development (UNCTAD) International Trade Center (ITC) na International Law Commission (ILC).

Hatua hiyo pia imehusisha mashirika makubwa yasiyo ya UN yakiwemo Jopo la Kimataifa la Mabadiliko ya Tabianchi (IPCC) Shirika la Kimataifa la Nishati Jadidifu (IRENA) pamoja na majukwaa mbalimbali yanayoshughulikia uhamiaji mapambano dhidi ya ugaidi na nishati safi.

Uamuzi huo unakuja wakati Rais Trump akikaribia kutimiza mwaka mmoja tangu kuanza kwa muhula wake wa pili madarakani. Tangu kurejea Ikulu tayari amechukua hatua za kujitoa katika Shirika la Afya Duniani (WHO) Mkataba wa Tabianchi wa Paris na UNESCO.

Wachambuzi wa siasa za kimataifa wanaonya kuwa hatua hiyo inaweza kuathiri ushirikiano wa kimataifa hususan katika masuala ya tabianchi, biashara na usalama wa dunia huku White House ikisisitiza kuwa maslahi ya Marekani ndiyo kipaumbele kikuu cha utawala wa sasa.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii