Ndoa iliyokuwa ikitazamwa kama mfano wa upendo wa kudumu imani na mshikamano wa kifamilia sasa imevunjika hadharani Kristy na Desmond Scott ambao ni wanandoa maarufu wa mitandao ya kijamii nchini Marekani wameingia rasmi katika mchakato wa talaka huku madai ya usaliti yakitajwa kuwa chanzo kikuu cha kuvunjika kwa ndoa yao.
Kwa zaidi ya miaka kumi wanandoa hao walijenga maisha ya ndoa sambamba na umaarufu mkubwa mtandaoni hasa kupitia TikTok, ambapo walikuwa wakishirikisha maudhui kuhusu ndoa, malezi ya watoto na changamoto za maisha ya kifamilia.
Video zao zilivutia mamilioni ya wafuasi waliowaona kama uthibitisho kwamba ndoa ya muda mrefu inaweza kudumu hata katika zama za mitandao ya kijamii.
Tofauti na wanandoa wengi wa mitandaoni Kristy na Desmond walijijengea jina kwa kuonyesha maisha halisi bila kupamba sana. Walizungumza wazi kuhusu majukumu ya ndoa mawasiliano na kujifunza kutokana na makosa hali iliyowafanya waonekane kuwa wa karibu na maisha ya watu wa kawaida.
Umaarufu huo uliwafanya mashabiki wengi kujihisi kama sehemu ya familia yao, jambo lililoongeza uzito wa kihisia pale taarifa za talaka zilipoanza kusambaa.
Hatua ya kuvunjika kwa ndoa ilithibitishwa pale Kristy Scott alipofungua kesi ya talaka, akieleza katika nyaraka za kisheria kuwa ndoa ilikuwa “imevunjika kabisa” kufuatia kupotea kwa imani, huku madai ya kutokuwa mwaminifu yakitajwa kama sababu kuu.
Uamuzi huo ulizua mjadala mpana miongoni mwa mashabiki, wengi wao wakijiuliza kama usaliti huo ndio uliovunja ndoa, au ulikuwa ni kilele cha changamoto zilizokuwa zikijitokeza kwa muda mrefu.
Kauli ya Kristy: “Nilichagua Amani Badala ya Maumivu”Baada ya habari za talaka kusambaa, Kristy alizungumza moja kwa moja kupitia video ya TikTok iliyosambaa kwa kasi, akifunguka kuhusu maumivu aliyopitia.
“Sikuwahi kufikiria ningefika hatua hii,” alisema Kristy, akisisitiza kuwa uamuzi wa kuvunja ndoa haukuwa mwepesi.
Aliongeza kuwa alilazimika kuchagua “amani badala ya maumivu” na kuweka mbele usalama wa kihisia wake na wa watoto wake.
Hadi sasa, Desmond Scott bado hajatoa kauli ya kina kuhusu madai hayo, jambo linaloacha maswali mengi kwa umma.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime