Wanafunzi nchini Iran walifanya maandamano mitaani mjini Tehran Jumanne, siku moja baada ya wafanyabiashara wa mji huo mkuu kuandamana kupinga hali ya mbaya ya kiuchumi.
Kulingana na Ilna shirika la habari linalohusiana na harakati za wafanyakazi nchini Iran, maandamano yalizuka katika vyuo vikuu 10 kote nchini, vikiwemo saba huko Tehran ambavyo ni miongoni mwa vyuo vya kifahari zaidi nchini humo.
Siku ya Jumanne, vikosi vya usalama na polisi wa kupambana na ghasia waliwekwa katika sehemu kadhaa za makutano makubwa mjini Tehran na karibu na baadhi ya vyuo vikuu, huku baadhi ya maduka yaliyofungwa siku iliyopita katikati mwa mji mkuu yakifunguliwa tena.
Hatua hiyo ya wanafunzi ilijiri baada ya maandamano ya Jumatatu katikati mwa Tehran yaliyofanywa na wamiliki wa maduka, na siku moja kabla ya kufungwa kwa muda kwa benki, shule na biashara nyingine katika mji huo mkuu na katika majimbo mengi ili kuokoa nishati wakati wa hali ya hewa kali ya baridi.
Rais Masoud Pezeshkian -- ambaye ana mamlaka machache chini ya mfumo wa serikali wa Iran kuliko kiongozi mkuu Ayatollah Ali Khamenei -- alikutana Jumanne na viongozi wa wafanyakazi na kutoa mapendekezo ya kukabiliana na mgogoro wa kiuchumi, kulingana na shirika la habari la Mehr.
Uchumi wa nchi hiyo, ambao tayari umeathiriwa pakubwa na miongo kadhaa ya vikwazo vya Magharibi, ulizidi kuwa mbaya baada ya Umoja wa Mataifa mwishoni mwa Septemba kurejesha vikwazo vya kimataifa vilivyohusishwa na mpango wa nyuklia wa nchi hiyo ambavyo viliondolewa miaka 10 iliyopita.