EU yajiandaa kuweka vikwazo vipya dhidi ya Iran

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, amesema Umoja huo unajiandaa kuweka vikwazo vipya dhidi ya Iran.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema Umoja huo unajiandaa kuweka vikwazo vipya dhidi ya Iran, huku idadi ya vifo vinavyotokana na ukandamizaji wa maandamano ya kuipinga serikali ikizidi kuongezeka.

Von der Leyen amelaani matumizi ya nguvu kupita kiasi na hatua za kuendelea kukandamiza uhuru wa raia.

Kupitia mitandao ya kijamii, ameandika kuwa ameshtushwa na idadi kubwa ya vifo na kusisitiza kuwa Umoja wa Ulaya EU inasimama na wananchi wa Iran wanaopigania uhuru wao.

Paula Pinho ni msemaji wa Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen.

"Tayari kuna msimamo ulio wazi kuhusu hili, kutoka upande wetu na pia kutoka kwa von der Leyen. Tunaangalia uwezekano wa kuweka vikwazo zaidi."

Kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za binadamu lenye makao yake Oslo, Iran Human Rights (IHRNGO), takriban watu 648 wameuawa tangu maandamano yalipoanza mwezi Desemba. Makadirio mengine yanaonyesha idadi hiyo inaweza kuzidi 6,000, huku zaidi ya 10,000 wakiaminika kukamatwa.

Iran imekumbwa na maandamano makubwa tangu Disemba 28. Kilichoanza kama malalamiko ya wafanyabiashara kuhusu kushuka kwa thamani ya riale na hali ngumu ya kiuchumi, kimegeuka na kuwa maandamano ya kitaifa dhidi ya utawala wa nchi hiyo.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii