Rais wa Angola Joao Lourenco ambaye pia ni mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) alikutana na viongozi wa kidini kutoka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mjini Luanda siku ya Jumatano kujadili hali ya usalama mashariki mwa DRC.
Mkutano huo mjini Luanda ulijumuisha wachungaji kutoka muungano wa Maaskofu wa kanisa katoliki nchini DRC CENCO na wachungaji kutoka makanisa mengine kufuatia mwaliko wa Angola.
Mkutano huu unakuja siku chache baada ya safari mbili chini ya wiki moja zake Rais wa DRC Félix Tshisekedi kwenda Luanda kwa mashauriano na mwenzake wa Angola kuhusu mzozo huo.
Mazungumzo haya yanajiri wakati mazungumzo juu ya itifaki sita zinazonuiwa kukamilisha makubaliano mawili ya kwanza ya amani kati ya serikali ya Kongo na waasi wa AFC/M23 yakikwama kulingana na vyanzo vya habari.
Baada ya kutangaza kujiondoa katika jukumu la upatanishi katika mgogoro wa Kongo mwezi Machi mwaka uliopita Angola inaonekana kurejelea jukumu hilo taratibu huku ikifanya mashauriano na washikadau mbalimbali.