Mkuu wa Mipango Mbogwe Afikishwa Baraza la Maadili

Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imemfikisha mbele ya Baraza la Maadili Mkuu wa Idara ya Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita Alex Manyama kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka.

Manyama anayekabiliwa na mashtaka manne alifikishwa mbele ya Baraza hilo Januari 14, 2026 katika ukumbi wa Ofisi za Sekretarieti ya Maadili jijini Dodoma kujibu tuhuma dhidi yake ambazo kwa pamoja alizikiri.

Wakili Mkuu wa Serikali.Hassan Mayunga alieleza kuwa mlalamikiwa alishindwa kutimiza matakwa ya kifungu cha 6(1)(a) na 6(1)(c) vya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma hivyo kukiuka maadili ya uongozi kwa mujibu wa kifungu cha 6(2) cha sheria hiyo.

Mayunga alisema kuwa Manyama alipokuwa akikaimu nafasi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbogwe aliwahamisha watumishi Asifiwe Chipata na Mercy Kabaka na kuwashusha vyeo bila kufuata sheria kanuni na taratibu za utumishi wa umma.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka vitendo hivyo vilikiuka pia Kanuni ya 3(2)(a) ya Kanuni za Udhibiti wa Mgongano wa Maslahi.

Baada ya kusomewa mashtaka Mwenyekiti wa Baraza la Maadili Jaji mstaafu Rose Teemba alimuuliza mlalamikiwa kama anakiri makosa hayo ambapo Manyama alikiri na kuomba asamehewe akidai alikosa umakini katika utekelezaji wa majukumu aliyopewa.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii