Watu kadhaa wamefariki na wengine kujeruhiwa siku ya Jumapili, Januari 18, kusini mwa Uhispania, msemaji wa kikosi jamii, Guardia Civil, ametangaza, wakati treni ilipoacha njia yake na kugongana na treni nyingine, na kusababisha treni hiyo kuacha njia yake. Huduma za usafiri wa treni za mwendo kasi zimesitishwa angalau hadi Jumatatu, Januari 19, kati ya Madrid na miji kusini mwa nchi.
Treni mbili za mwendo kasi ziliacha njia usiku wa Jumapili, Januari 18 kuamkia Jumatatu Januari 19 kusini mwa Uhispania, imetangaza Adif, kampuni inayosimamia huduma za usafiri wa treni za mwendo kasi. Angalau watu 21 wamefariki katika ajali hiyo, kulingana na ripoti ya awali iliyotolewa na Guardia Civil. Watu thelathini wamelazwa hospitalini wakiwa katika hali mbaya, Waziri wa Uchukuzi ametangaza usiku wa kuamkia leo Jumatatu.
Watu wapatao 300 walikuwa ndani ya treni hizo, kulingana na wenzetu wa El País. Mamlaka za kikanda za Andalusia zinaripoti angalau majeruhi 73 na "usiku ambao unaonekana kuwa mgumu." Waziri wa Uchukuzi wa Uhispania Oscar Puente ameonya kwenye mitandao ya kijamii kwamba "athari ilikuwa mbaya sana" na kwamba idadi ya vifo inaweza kuongezeka kutokana na "taarifa za kutisha" kuhusu ajali hiyo.
Ajali hiyo ilitokea karibu na Adamuz, si mbali na Cordoba. "Treni ya Iryo 6189 Málaga-Madrid iliacha njia huko Adamuz na kusimama kwenye reli iliyo karibu.
Treni ya Madrid-Huelva, iliyokuwa ikisafiri kwenye njia hiyo, pia iliacha njia," Adif, imesema katika ujumbe uliotumwa kwenye mitandao ya kijamii.
Walioshuhudia wanasema treni hiyo ilitetemeka kwa nguvu kabla ya kuacha njia na kwamba hali ilikuwa mbaya, haswa kwa mabehewa 6, 7, na 8, anaripoti mwandishi wetu huko Madrid, François Musseau. Treni hiyo iliyofanya ajali, ilipoteza njia na kujikuta kwenye njia nyingine, na hivyo kusababisha treni nyingine iliyokuwa ikisafiri upande mwingine, kutoka Madrid hadi Andalusia, kupoteza njia.
Adif imesema kwamba ajali hiyo ilitokea takriban dakika kumi baada ya treni ya Iryo kuondoka Malaga kuelekea Madrid saa 12:40 jioni saa za Uhispania.