VIONGOZI wote wa Serikali ya Kijiji cha Namwanga Kata ya Hezya Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe wamejiuzulu nyadhifa zao kwa pamoja wakilalamikia kile walichokitaja kuwa ni ukandamizaji na udhalilishaji kutoka kwa viongozi wa ngazi ya kata.
Uamuzi huo umefikiwa Januari 17 mwaka huu na kutangazwa rasmi Januari 20 mwaka huu na Mwenyekiti wa kijiji hicho Japhet Mbukwa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya viongozi wenzake.
Mbukwa amesema hatua yao imekuja siku chache baada ya yeye kukamatwa na Jeshi la Polisi kwa amri ya Mtendaji wa Kata ya Hezya Ibrahim Tusamare jambo ambalo viongozi hao wanalidai kuwa ni sehemu ya manyanyaso dhidi yao.
Ameeleza kuwa mbali na kukamatwa kwake mabalozi watatu wa kijiji hicho wanaendelea kusakwa na polisi kwa tuhuma za kuhusika katika uharibifu wa mazingira ikiwemo madai ya kuwaruhusu raia kutoka Malawi kujihusisha na biashara haramu ya uchomaji mkaa.
Hata hivyo Mbukwa amekanusha vikali tuhuma hizo akisisitiza kuwa hakuna uamuzi wa serikali ya kijiji uliowahi kuwaruhusu wageni kuharibu mazingira na kwamba raia wa Malawi anayetajwa aliishi katika kijiji hicho muda mrefu kabla hajachaguliwa kuwa mwenyekiti.
Kwa upande wake Mtendaji wa Kata ya Hezya Ibrahim Tusamare amesema kwa njia ya simu kuwa alitoa amri ya kukamatwa kwa Mwenyekiti wa kijiji hicho pamoja na raia wa Malawi kutokana na tuhuma za kuhusika katika vitendo vya uharibifu wa mazingira ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Namwanga.
Aidha amefafanua kuwa hifadhi hiyo inayozungukwa na vijiji vinne imekuwa ikivamiwa na watu wanaojihusisha na ukataji miti na uchomaji mkaa kinyume cha sheria hivyo hatua za kisheria zililazimika kuchukuliwa.
Hata hivyo tukio hilo limeibua mjadala mkubwa kuhusu mahusiano kati ya viongozi wa vijiji na ngazi ya kata pamoja na usimamizi wa rasilimali za mazingira katika Wilaya ya Mbozi.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime