Marekani kutofungua mashitaka kashfa ya Nyaraka za Epstein

Licha ya ugunduzi mkubwa ulioibuliwa kwenye kile kiitwacho Nyaraka za Epstein Naibu Mwanasheria Mkuu wa Marekani, Todd Blanche ameondosha uwezekano wa kufunguwa mashitaka ya uhalifu kwa wale waliotajwa.

Naibu Mwanasheria huyo alisema siku ya Jumapili (Februari 1) kwamba msimamo wa wizara yake unasalia kuwa ule ule uliotolewa majira ya kiangazi kwamba hakuna cha kushitakiwa kwenye nyaraka hizo.

Siku ya Ijumaa (Januari 30) wizara hiyo ilichapisha rundo la nyaraka ambalo limerejesha upya tuhuma za mahusiano kati ya muhalifu huyo wa ngono kwa watoto wadogo na watu kadhaa wenye vyeo na majina makubwa ndani na nje ya Marekani.

Miongoni mwa wanaotajwa kwenye nyaraka hizo ni aliyekuwa mwanamfalme wa Uingereza, Andrew, mabilionea Elon Musk, Bill Gates, rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton, na hata rais wa sasa, Donald Trump, na waziri mkuu wa zamani wa Israel, Ehud Barak.

Jeffrey Epstein alikufia gerezani mwaka 2019 alikokuwa akingojea hukumu yake kwa uhalifu wa ngono kwa watoto, ubakaji, na usafirishaji haramu wa binaadamu.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii