Kifo cha Saif al-Islam Gaddafi

Saif al-Islam Gaddafi, mtotoa mdogo wa Muammar al-Gaddafi na mgombea katika uchaguzi wa rais wa 2021, ambao hatimaye haukufanyika, ameuawa nyumbani kwake Zintan, jiji lililoko kaskazini magharibi mwa Libya, siku ya Jumanne, Februari 3. Ndugu zake wamethibitisha kifo chake nyumbani kwake. Kwa muda mrefu akichukuliwa kuwa mrithi wa baba yake, alikuwa na umri wa miaka 53.

Kulingana na wasaidizi wake, watu wanne wenye bunduki wasiojulikana walivamia nyumba yake na kumpiga risasi na kufa papo hapo. Tangu alipoachiliwa kutoka gerezani mwaka wa 2016, Saif al-Islam alikuwa akiishi kwa kujificha huko Zintan, akiwa na wafanyakazi wawili pekee, katika nyumba ya pekee kwenye mteremko wa mlima unaopakana na Jangwa la Hamada.

Kwa sababu za usalama, aliishi maisha ya kujificha na aliwasiliana tu na watu wachache sana, "wanaohesabika kwa vidole vya mkono mmoja," inasemekana.

Chini ya utawala wa baba yake, Muammar Gaddafi, Saif al-Islam alijijengea taswira kama mwanamageuzi. Akiwa amesoma London, alizungumza Kiingereza vizuri na alicheza nafasi ya mpatanishi katika misheni nyeti za kidiplomasia, kama vile mazungumzo kuhusu Libya kuachana na silaha za maangamizi.

Saif al-Islam akawa mzungumzaji anayependelewa na Magharibi, akitaka kupitishwa kwa katiba na kuheshimiwa kwa haki za binadamu. Katika miaka ya 2000, alichangia kuachiliwa kwa wafungwa wa kisiasa, wakiwemo Waislamu, na akaanzisha mradi wa mageuzi uliolenga kuiweka Libya kwenye njia ya demokrasia, lakini alijikuta na anakabiliana na upinzani kutoka walinzi wa zamani wa utawala - na hatimaye akashindwa.

Lakini mwanzoni mwa uasi dhidi ya utawala wa baba yake mnamo mwaka 2011, aliahidi "kumwaga damu," na kuvunja sifa yake kama mwanamageuzi. Alikamatwa alipokuwa akijaribu kukimbia na kisha akakaa kizuizini kwa miaka sita huko Zintan, akiwa ametengwa karibu kabisa. Alihukumiwa kifo mwaka wa 2015 baada ya kesi kabla ya kupewa msamaha.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii