Serikali ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga imeendelea kulitambua zao la pamba kama zao la kimkakati kutokana na mchango wake mkubwa katika uchumi wa mkulima na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa katika kikao maalumu cha Kamati ya Mazao wilayani Kishapu, kilicholenga kusikiliza changamoto za zao la pamba na kuweka mikakati ya kuzitatua ili kilimo hicho kiwe na tija kwa wakulima.
Akizungumza wakati wa kufungua kikao hicho, Ofisa Tawala wa Wilaya ya Kishapu, Fadhili Mvanga, akimwakilisha Mkuu wa Wilaya, Peter Masindi, amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wa kulirejesha zao la pamba katika hadhi yake ya kuinua uchumi wa mkulima.
Mvanga amesema Serikali inalenga kuimarisha mifumo ya uzalishaji wa pamba, kuhakikisha upatikanaji wa pembejeo kwa wakati, kutoa elimu ya kilimo chenye tija pamoja na kusimamia masoko ili mkulima anufaike ipasavyo.
“Ili kufikia dhamira ya kurejesha hadhi ya zao la pamba, lazima kuwepo na ufuatiliaji wa karibu kati ya maofisa ugani na wakulima, ikiwemo kuwafikia mashambani na kuwapa elimu ya vitendo ya kilimo chenye tija,” amesema Mvanga.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Josephat Limbe, amesema changamoto ya bei isiyoridhisha imekuwa ikiwakatisha tamaa wakulima wengi, hali inayodhoofisha mchango wa zao hilo katika maisha yao ya kiuchumi.
Ameomba kuwepo kwa soko huria la pamba wilayani humo badala ya mnunuzi mmoja, ili kuongeza ushindani wa bei na kumuinua mkulima.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba Tanzania, Marco Mtunga, amesema Serikali inaendelea kuboresha sera, usimamizi na ushirikiano na wadau wa pamba kwa lengo la kuimarisha masoko na kumlinda mkulima dhidi ya changamoto za bei.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime