Nyumba 3,000 kando ya Mto Msimbazi kubomolewa

Nyumba zaidi ya 3,000 zilizopo kandokando ya Mto Msimbazi zinatarajia kubomolewa ili kupunguza athari za mafuriko katika eneo la Jangwani na kuboresha mipango miji.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Reuben Kwagilwa ameeleza hayo leo Februari 05 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Kinondoni, Abbas Tarimba, aliyetaka kujua lini Mradi wa Bonde la Mto Msimbazi utaanza na kukamilika.

Akijibu swali hilo Kwagilwa, amesema mradi huo unalenga kupunguza athari za mafuriko katika eneo la Jangwani na kuboresha mipango miji katika eneo la chini la bonde, kwamba kati ya nyumba 3,000 zitakazobomolewa, 2,500 zimeshalipwa fidia.

Amesema, mradi ulianza kutekelezwa rasmi Februari, 2023 na utatekelezwa kwa muda wa miaka sita.

“Mradi unatarajia kuhamisha nyumba zaidi ya 3,000 ambapo hadi sasa nyumba 2,500 zimeshalipwa fidia na kuhama eneo la mradi. Mradi unatarajia kupanua na kuongeza kina cha Mto Msimbazi pamoja na kuongeza uwezo wa mawanda ya mafuriko katika eneo la chini la bonde,”amesema.

Aidha, amesema udongo utakaotokana na upanuzi huo utatumika kutengeneza maeneo salama kwa makazi na biashara pembezoni mwa bonde.

“Jumla ya hekta 57 zinatarajiwa kupatikana kwa matumizi hayo. Mkataba wa ujenzi huu unatarajiwa kusainiwa Februari, 2026 na kazi kuanza rasmi ifikapo Mei, 2026,”amesema.

Amesema mradi huo unajenga daraja jipya eneo la Jangwani lenye urefu wa mita 390 chini ya usimamizi wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kazi hiyo imeanza tangu Mei, 2025 na ujenzi umefikia asilimia 15.

Amesema, mradi utajenga karakana mpya ya mabasi ya mwendokasi katika eneo la Ubungo Maziwa, mkataba wa kazi hiyo unatarajiwa kusainiwa Februari, 2026.

Amesema mradi unatarajiwa kuboresha maeneo korofi katika eneo la juu la bonde pamoja na kuratibu shughuli za kibinadamu, ili kudhibiti mmomonyoko wa udongo unaotuama eneo la chini na kusababisha mafuriko.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii