Watu wasiopungua wanane waliuawa katika ajali ya treni ya mizigo iliyotokea kusini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wamesema maafisa wa eneo hilo. Afisa wa habari wa ofisi ya mkoa wa Lualaba, Josue Muyumba amesema ajali hiyo iliyotokea usiku wa kuamkia Jumapili katika kijiji cha Buyofwe, vile vile iliwajeruhi watu wengine 20. Katikati mwa mwezi Machi, treni nyingine ilianguka katika kijiji hicho hicho, na kuuwa watu 75 na kuwajeruhi wengine 125. Gavana wa mkoa wa Lualaba Deoda Kapenda amesema yumkini idadi ya waliouawa katika ajali hii ya Jumapili ni kubwa zaidi, kwa sababu watu wengi husafiri kwa kujificha katika mizigo, na huenda wamenaswa chini ya mabehewa yaliyopinduka. Ajali za treni ni matukio ya mara kwa mara nchini Kongo, kutokana na uhaba wa treni za abiria na uchakavu wa reli.