Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
(TMA) imekutana na waandishi wa habari kujadili athari za mabadiliko ya
tabia nchi katika mifumo ya hali ya hewa ikiwa ni maandalizi ya kurejea
utabiri wa MASIKA uliotolewa Februari 2022.
Akizungumza na
waandishi wa habari, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa tatu wa Rais wa
Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi, amesema
mifumo ya hali ya hali ya hewa imebadilika kutokana na mabadiliko ya
tabia nchi yaliyopelekea kubadilika kwa mwenendo mzima wa mvua za msimu
wa MASIKA 2022.
Aliyazungumza hayo alipokuwa akifungua warsha ya
wanahabari iliyofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya
TMA, Ghorofa ya tatu, Ubungo Plaza, April 12,2022.
“Tanzania
tumeanza kuziona athari za mabadiliko ya tabia nchi, katika mifumo ya
hali ya hewa hasa kubadilika kwa joto la bahari ambalo kwa kawaida
halibadiliki kwa haraka kutokana na tabia ya maji kutunza joto lake kwa
muda mrefu.” Alisema Dkt. Kijazi.
Dkt. Kijazi alisema kuongezeka
kwa joto duniani (global warming) kunasababisha kuyeyuka kwa barafu
zilizoko katika ncha za dunia na hivyo kuongeza vina vya bahari katika
maeneo mbalimbali duniani ikiwa Pamoja na kubadilika kwa hali ya joto la
bahari na hivyo kuathiri mifumo ya hali ya hewa.
Aidha Dkt.
Zewdu Segele ambaye ni mtaalam wa masuala ya hali hewa kutoka kituo cha
utabiri na matumizi ya hali hewa (ICPAC) alisema, ICPAC imetoa mrejeo wa
utabiri wake wa Machi – Mei ambao iliutoa mwezi Februari. Dkt. Zewdu
alisema mifumo ya awali ilionyesha uwepo wa mvua za juu ya wastani
katika nchi za pembe ya Afrika ikiwemo Tanzania, lakini baada ya mifumo
kubadilika nchi hizo sasa zitapata mvua za chini ya wastani.
Dkt.
Zewdu aliongeza kusema utabiri unaotolewa na ICPAC ni wa maeneo makubwa
hivyo nchi wanachama wana jukumu la kuandaa utabiri wa maeneo madogo
madogo katika nchi zao.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
inatarajia kutoa rasmi mrejeo wa utabiri wa mvua za msimu wa Masika
(MAM) 2022 leo tarehe 13/04/2022.