ais wa Tanzaniza, Samia Suluhu Hassan amezindua rasmi nembo ya sensa na kutangaza siku ya sensa ya watu na makazi itakuwa Jumanne Agosti 23, 2022.
Rais Samia amefanya uzinduzi wa nembo hiyo na kutangaza siku hiyo ya sensa leo Ijumaa Aprili 8, 2022 katika hoteli ya Golden Tulip mjini Unguja, Zanzibar.
Rais Samia amesema shughuli ya uhesabuji watu inaisaidia Serikali kupanga vyema mipango yake ya maendeleo.
"Hili sio jambo geni kwa hiyo ni muhimu na tujitahidi kukamilisha mipango hii kwa manufaa ya Taifa letu," amesema
Rais Samia ameagiza nembo hiyo itumike kwa shughuli zote za kiserikali na taasisi binafsi ili kuhamasisha wananchi waweze kutambua umuhimu wa kihesabiwa.
"Kwa taasisi za Serikali nembo hii iwekwe kwenye machapisho, website na mitandao ya kijamii lakini kwa upande wa taasisi binafsi zinaweza kuwekwa hata kwenye vifungashio au risiti na tiketi, kikubwa kila sehemu tuone hiyo nembo," amesema Rais Samia
Awali Mwenyekiti wa kamati ya sensa ambaye pia ni Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema siku ya sensa imepangwa kwa kuzingatia maombi ya viongozi wa dini isiwe siku ya ibada.
Majaliwa amesema mpaka sasa maandalizi ya shughuli hiyo ya sensa yamefikia asilimia 79 na kwamba kazi hiyo inaendelea kuratibiwa kwa ushirikiano mkubwa kati ya Serikali zote mbili; Serikali ya Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibari.