FISI ASHAMBULIA MTOTO WA MIAKA SITA BARIADI

Mtoto Spora Sambalya mwenye miaka sita (6) na mwanafunzi wa darasa la awali Shule ya Msingi Kidinda mkoani Simiyu amenusurika kifo baada ya kushambuliwa na fisi majira ya saa moja asubuhi akiwa njiani kuelekea shule.

Tukio hilo limetokea katika Mtaa wa Nyangaka ambapo mwananchi mmoja aliyekuwa akielekea kwenye shughuli zake shambani alimuokoa mtoto huyo huku akiwa tayari amejeruhiwa maeneo ya kichwani.

Shuhuda wa tukio hilo Gimbuya Jidana amesema, alimuona fisi huyo na muda mfupi baadaye walitokea watoto wanne waliokuwa wakielekea shule na mara fisi huyo alianza kuwakimbiza na kufanikiwa kumkamata mtoto mmoja aliyeanguka wakati akijaribu kujiokoa.

Gimbuya amesema alitumia panga kumtoa fisi huyo na kufanikiwa kumuokoa mtoto huyo akiwa amejuruhiwa maeneo ya kisogoni.

Mganga mkuu wa Mji wa Bariadi, Dkt. Judith Ringia amethibitisha kumpokea mtoto huyo katika Hospitali ya Bariadi ambapo wataalam wamempatia matibabu na hali yake imeendelea kuimarika.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii