Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
CITI
BANK imeahidi kuisaidia Tanzania kupata mikopo yenye masharti nafuu
kutoka katika Benki hiyo pamoja na washirika wake kwa ajili ya
utekelezaji wa miradi ya kimkakati ukiwemo mradi wa ujenzi wa Reli ya
Kisasa (SGR) pamoja na kuahidi kuwa balozi wa kutafuta wawekezaji
wataowekeza mitaji na teknolojia hapa nchini.
Ahadi hiyo
imetolewa Jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa wa Benki hiyo anayesimamia
nchi za Afrika-Kusini mwa Jangwa la Sahara, Bw. Akinsowon Dawodu,
alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango
Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb).
“Nafahamu Serikali
inauhitaji mkubwa wa ujenzi wa miundombinu ukiwemo mradi wa Reli ya
Kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza kuelekea nchi za Rwanda, Burundi
na DRC- Congo, nasi tumeleta andiko letu serikalini, tunataka kusaidia
kupatikana kwa fedha kutoka katika taasisi za fedha za kikanda na
kimataifa kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo uuzwaji wa hatifungani”
alisema Bw. Dawodu.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki
hiyo hapa nchini, Bw. Geofrey Mchangila, alisema kuwa Citi Bank imekuwa
ikifanya shughuli zake za kibenki hapa nchini kwa zaidi ya miaka 27 na
kwamba malengo ya kutaka kufanyakazi na Serikali katika kutafuta
rasilimali fedha na kwamba watahakikisha wanatafuta na kutoa mikopo
yenye riba nafuu.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa, Dkt.
Mwigulu Lameck Nchemba, aliishukuru Benki hiyo kwa kuwasilisha
mapendekezo yake serikalini kuhusu namna ya kufanikisha ujenzi wa mradi
mkubwa wa Reli ya Kisasa ambao utakuwa na manufaa makubwa kiuchumi si tu
kwa Tanzania, bali nchi nyingine zinazopakana na Tanzania ambazo
hazipakani na Bahari.
Alieleza kuwa Mkandarasi atakayejenga
kipande cha Reli ya Kisasa kutoka Makutupora ya mkoani Singida hadi
mkoani Tabora amepatikana na mkandarasi atayejenga reli hiyo kutoka
Isaka hadi Mwanza yuko katika eneo la mradi na Mkandarasi atakayejenga
reli kuanzia Isaka hadi Tabora atapatikana muda si mrefu kuanzaia sasa.
“Dira
ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ni kuona kuwa Reli ya Kisasa ya kuanzia Makutopora (Singida)
hadi Mpaka Mwanza na kuanzia Tabora hadi Kigoma, ijengwe sambamba na kwa
kasi, wakati huohuo Reli ya Kusini mwa Tanzania kutoka Bandari ya
Mtwara hadi Mbamba bay kuelekea nchi za SADC zilizoko ukanda huo ziweze
kufikiwa na reli hiyo” alieleza Dkt. Nchemba
Aidha, Dkt. Nchemba
aliushukuru uongozi wa Benki hiyo kwa kuamua kuwa balozi wa Tanzania
katika kutafuta wawekezaji wataowekeza mitaji na teknolojia na kwamba
Tanzania ni mahali salama pa kuwekeza kutokana mambo kadhaa ikiwemo
uwepo wa amani na utulivu, uwepo wa soko la uhakika la kikanda pamoja na
soko la ndani linalokua kwa kasi.
“Tanzania ina faida kuliko
nchi nyingi za Afrika ambapo kijiografia ni lango la zaidi ya nchi 7
ambazo hazina lango la Bahari na uwepo wa amani isiyolinganishwa na
nchini nyingi za Afrika ni kivutio cha mwekezaji yeyote na wanaweza
kulifikia robo au robo tatu ya soko la Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la
Sahara” alieleza Dk. Nchemba.
Alibainisha kuwa Tanzania ina idadi
kubwa ya watu hivyo kuwa na soko la uhakika la ndani linalokua kwa kasi
na uchumi wake hauyumbi akitolea mfano wakati wa Janga la Uviko-19
ambapo nchi nyingi ziliyumba kiuchumi lakini Tanzania uchumi wake
uliendelea kukua kwa kiwango chanya.
Mkutano huo wa Ujumbe wa
Citi Bank na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu
Nchemba, ulihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Hamad
Hassan Chande, Naibu Katibu Mkuu Bw. Lawrence Mafuru, Kamishna wa Idara
ya Madeni Justine Japhet, Kaimu Kamishna wa Sera Bw. Wiiliam Mhoja na
Maafisa Wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha na Mipango.