Mbunge wa Ilemela agawa pikipiki kwa vijana

Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Kafiti Wilium Kafiti, ametoa msaada wa pikipiki 100 kwa vijana wa Mkoa wa Mwanza katika tukio lililovuta hisia na kuacha alama chanya kwa jamii. 

Hafla hiyo imefanyika kwa lengo la kuwawezesha vijana kiuchumi, hasa wanaojihusisha na shughuli za ujasiriamali na usafirishaji, ili kuongeza kipato na kujiajiri kwa njia halali na endelevu.

Akizungumza wakati wa tukio hilo, Mbunge Kafiti amesisitiza kuwa uwezeshaji wa vijana ni msingi wa maendeleo ya kweli, akieleza kuwa pikipiki hizo ni chachu ya kubadili maisha

 Amehimiza vijana kuzitumia kwa nidhamu, uaminifu na kufuata sheria za usalama barabarani, huku akiahidi kuwa zoezi hilo la kutoa pikipiki kwa vijana litafika na wilaya jirani pia ili kuwasaidia vijana wote wa Mwanza.

Kwa upande wa vijana walionufaika wameonesha shukrani zao kwa hatua hiyo, wakisema imewapa matumaini mapya na ari ya kufanya kazi kwa bidii.

Tukio hili limepokelewa kwa hisia mseto za furaha na matumaini, likitafsiriwa kama mfano wa uongozi unaogusa maisha ya wananchi moja kwa moja na kuimarisha mshikamano kati ya viongozi na jamii wanayoihudumia.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, ameshiriki kikamilifu zoezi la ugawaji wa pikipiki kwa vijana, akieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kuwajengea vijana uwezo wa kujitegemea kiuchumi.

 Amepongeza juhudi za Mbunge wa Ilemela kwa kugusa maisha ya vijana moja kwa moja, huku akisisitiza kuwa fursa hizo zinapaswa kutumiwa kwa malengo chanya ya kujiletea maendeleo binafsi na kuchangia ustawi wa jamii kwa ujumla.

Aidha, Mkuu wa Mkoa amewataka vijana kuepuka vitendo vyovyote vinavyoweza kuvuruga amani na utulivu wa Mkoa wa Mwanza, akisisitiza kuwa maendeleo hayawezi kupatikana pasipo amani.

 Amehimiza uzalendo, utii wa sheria na kushiriki katika shughuli halali za kiuchumi, akieleza kuwa serikali itaendelea kuwaunga mkono vijana wanaochagua njia sahihi za kujijenga na kuijenga nchi.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii