Raia nchini Japan, wamepiga kura Jumapili katika uchaguzi unaotazamiwa kukipa ushindi wa kihistoria chama cha Waziri Mkuu Sanae Takaichi.
Kulingana na utafiti uliohusisha kura ya maoni uliofanyika mara kadhaa nchini Japan, Chama cha Takaichi cha Liberal Democratic (LDP) ambacho kimeongoza kwa miaka mingi kinatabiriwa kupata viti visivyopungua 233 katika bunge lenye jumla ya viti 465. Pamoja na kiwango kikubwa cha theluji katika miji mingi ukiwemo mji mkuu Tokyo, raia wamejitokeza kushiriki uchaguzi huo.
Licha ya kauli tata dhidi ya China, Takaichi anazidi kuungwa mkono
Waziri Mkuu Takaichi anaungwa mkono kwa kiasi kikubwa nchini mwake licha ya kauli yake ya hivi karibuni iliyozua mzozo wa Kidiplomasia kuwa, Japan inaweza kuishambulia kijeshi China kama ikiishambulia Taiwan.
Ikiwa chama chake kitapata ushindi mkubwa katika uchaguzi huu, Waziri Mkuu huyo wa Japan huenda akaliongoza taifa hilo hadi mwaka 2028.