Afrika Kusini yatangaza kuwaondoa wanajeshi wake Kongo

Afrika Kusini imetangaza Jumamosi kuwa itawaondoa wanajeshi wake ambao ni sehemu ya Ujumbe wa Kulinda Amani wa Umoja wa Mataifa ulio nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Hayo ni kulingana na taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Rais Cyril Ramaphosa. Taarifa hiyo imesema Ramaphosa amemwambia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kuwa, uamuzi huo umetokana na haja ya kuvifanyia mageuzi vikosi vya ulinzi vya Afrika Kusini.

Nchi hiyo imekuwa ikishiriki katika juhudi za kulinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa miaka 27.

Afrika Kusini ina wanajeshi 700 katika kikosi cha Umoja wa Mataifa Kongo

Wanajeshi wake 700 ni sehemu ya ujumbe wenye polisi na wanajeshi 11,000 wanaouwakilisha Umoja wa Mataifa, katika kupambana na makundi ya waasi yanayoendesha shughuli zake mashariki mwa Kongo.

Mchakato wa kuwaondoa wanjeshi hao wa Afrika Kusini nchini Kongo, utaratibiwa na Umoja wa Mataifa na unatarajiwa kukamilika kabla ya Desemba mwaka huu.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii