Mnamo tarehe 31/01/2022 majira ya saa
04:30 alfajiri huko Mtaa wa Hasanga uliopo Kata ya Uyole Tarafa ya
Iyunga Jijini Mbeya, mtu mmoja aitwaye JUSTIN NAMWINGA [55] Mwenyekiti
wa Mtaa wa Hasanga alikutwa akiwa ameuawa kwa kuchomwa kisu kifuani
chini ya titi la upande wa kushoto jirani na nyumbani kwake.
Awali
kabla ya tukio hilo, JUSTIN NAMWINGA [55] alikuwa amelala na familia
yake nyumbani kwake, walifika watu na kubisha hodi na kumjulisha kuwa
kuna wezi nje, hivyo alitoka ili kutoa msaada baada ya muda kidogo
majirani nao waliamka baada ya kusikia vishindo lakini walipofika nje
walimkuta marehemu amelala kifudifudi huku akitokwa damu nyingi kifuani.
Chanzo
cha tukio ni mapambano na wezi. Mwili wa marehemu umehifadhiwa
Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kwa uchunguzi wa kitabibu. Jeshi la
Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na msako mkali kuwabaini na kuwakamata
watuhumiwa wa tukio hili.
Aidha ninatoa rai kwa wananchi na
yeyote mwenye taarifa za mtu/watu au kikundi cha watu waliohusika kwenye
tukio hili watoe taarifa kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya ili
watuhumiwa wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.