Rais Samia Suluhu Hassan amesema Mkoa wa Mara una tatizo la kukwama kwa miradi jambo ambalo linahitaji kupatiwa ufumbuzi.
Ametoa kauli hiyo leo Jumapili Februari 6, 2022 kwenye hafla ya uwekaji jiwe la msingi mradi wa maji wa Mugango- Kiabakari wilayani Musoma huku akiahaidi kuzungumzia suala hilo katika mradi wa ujenzi wa hospitali ya rufaa ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere maarufu Kwangwa.
Mkuu huyo wa nchi ametolea mfano wa miradi iliyokwama kwa muda mrefu kuwa ni pamoja na hospitali hiyo ya rufaa iloyoanza kujengwa mwaka 1974 pamoja na mradi wa umwagiliaji wa Bugwema uliopo wilaya ya Musoma.
"Mkoa wa Mara una tatizo la kukwama kwa miradi mfano mzuri ni ile hospitali ya Mwalimu Nyerere iliyoanza kujengwa miaka ya 70 hadi Serikali ya awamu ya tano ilipoanza kutoa fedha kwaajili ya kuikwamua" amesema na kuongeza
Mradi mwingine nimeambiwa ni huo wa unwagiliaji wa Bugwema ambao na wenyewe nao umekwama kuanzia mwaka 1970 lakini niwaambie tunakwenda kufanyia kazi.
Amesema kuwa suluhisho la tatizo hilo atalitoa kwa manufaa ya wananchi na kwamba hali hiyo haikubaliki huku akisema kuwa inasikitisha kuona miradi ikikwama wakati wapo viongozi kuanzia ngazi ya mkoa hadi wilaya.
Rais Samia ameweka jiwe la msingi kwenye mradi wa maji wa Mugango-Kiabakari mradi unaotarajiwa kugharimu zaidi ya Sh70.5 bilioni hadi kukamilika.