Rais wa Urusi Vladmir Putin leo ameyasifu mahusiano ya karibu ya nchi yake na China, katika mkutano na mwenzake wa China, Xi Jinping, kabla ya kufunguliwa kwa Michezo ya Olimpiki ya majira ya Baridi mjini Beijing. Viongozi hao wawili wamekutana katika mji mkuu wa China wakati nchi zao zikilenga kuimarisha mahusiano huku zikikikabiliwa na ongezeko la ukosoaji kutoka nchi za Magharibi. Akizungumza kabla ya mkutano wao, Putin alisema Moscow imeandaa kandarasi mpya ya kusambaza gesi asilia ya mita za ujazo bilioni 10 nchini China kutoka Mashariki ya Mbali ya Urusi. Baadaye leo, rais huyo wa Urusi atashiriki katika sherehe za ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki. Beijing na Moscow wamelaani hatua ya nchi kadhaa ya kuisusia kidiplomasia michezo hiyo zikilalamikia kile serikali za Magharibi zinahoji kuwa ni ukiukaji mkubwa wa haki nchini China.