Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga amesema kuwa iwapo atachaguliwa kuwa rais katika uchaguzi mkuu wa Agosti, atahakikisha kuwa timu ya taifa ya soka Harambee Stars inashiriki katika mashindano ya mataifa ya Afrika (AFCON).
Akiipa hongera timu ya taifa ya Segenal kwa kushinda makala ya 33 ya mashindano hayo kwa kuinyuka Misri 4-2 kuptia mikwaju ya penalti baada ya sare ya 0-0 katika muda wa kawaida na ule wa ziada, Raila alisema soka itakuwa kuu miongoni mwa masuala atakayoangazia.
“Hongera Senegal kwa kushinda AFCON 2021. Ninaahidi kwa mashabiki wa soka nchini Kenya kuwa chini ya utawala wangu, Harambee Stars itakuwa katika makala ya AFCON yajayo,” Raila alisema kupitia mtandao wa Twitter.
Makala yajayo ya AFCON yataandaliwa nchini Ivory Coast mwaka 2023 ili kuhakikisha Kenya inashiriki, miongoni mwa masuala mengine, Raila alisema kuwa utawala wake utahakikisha kuwa klabu ndogo za jamii mbalimbali zinapigwa jeki na kuimarika.
“Tutawekeza katika soka tukaianza na klabu za mashinani na zile za jamii. Inawezekana,” aliongeza kiongozi huyo wa ODM.
Mwanzoni mwa makala ya 33 ya AFCON, Raila alipaza sauti yake kuhusu kukosekana kwa Kenya katika mashindano hayo huku mataifa madogo yakishamiri katika mashindano hayo.
“Visiwa vidogo kama Komoro na mataifa kama Burkina Faso yanacheza vizuri katika AFCON ilhali Kenya haipo. Kombe la dunia litakapochezwa, Kenya vilevile haitakuwepo,” Raila alisema katika mkutano wa kisiasa na jamii ya Maa mwezi Januari.
Waziri Mkuu huyo wa zamani aliapa kuwa chini ya serikali yake, Harambee Stars itapewa sapoti inayohitaji ili kuhakikisha kuwa ianafuzu mashindano mbalimbali kama kama kombe la dunia.
“Ninaahidi kuwa nikifika kule, Kenya itacheza AFCON na kombe la dunia,” alisema Raila.