Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia
Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amewapongeza Ngariba
waliokuwa wanajihusisha na vitendo vya ukeketaji baada ya kuacha kufanya
vitendo hivyo na kisha kugeuka kuwa wanaharakati wa kukemea vitendo
vinavyo dhalilisha utu wa mtoto wa kike na kumuachia maumivu makali.
Akifunga
Kongamano Maalum kwajili ya mapambano ya kutokomeza Ukeketaji
lilichofanyika mkoani Mara katika Wilaya ya Tarime, Dkt. Gwajima
alisema, kitendo cha Ngariba hao kuacha suala la Ukeketaji na kujiunga
na Serikali katika mapambano hayo ni ujasiri wa hali ya juu na nicha
kupongezwa.
“Mmewasikia wenyewe wakijieleza hapa, kwamba wapo
baadhi yao walikata shauri na kuacha kuendelea kukeketa, lazima
tuwapongeze sana kwa hatua hii. Lakini baadhi yao wanatishiwa hata
kutengwa na jamii zao baada ya kuacha vitendo hivyo vya kikatili, tuseme
kama Serikali na wadau tutakuwa nao bega kwa bega kuwatetea kwa nguvu
zote bila kuchoka” alisema Waziri Dkt. Gwajima.
Dkt. Gwajima
alisema dhana ya kwamba, mtoto kumvusha rika kutoka usichana kwenda kuwa
mama au mtu mzima sio lazima akeketwe zipo njia mbadala za kumvusha
binti rika ikiwepo kuwapatia mafunzo yakujitambua bila kumuathiri mwili
wake.
Ameongeza kuwa, zipo athari wanazo kumbana nazo Mabinti
wanaokeketwa ikiwepo athari za kisaikolojia na msongo wa mawazo, kwani,
vitendo hivyo hufanywa bila ridhaa ya wahusika, kupata maumivu makali,
kutokwa damu nyingi, kuuguza kidonda, changamoto za kujifungua na
uwezekano wa kupoteza maisha.
“Madhila mengine kusababisha
maambukizi ya magonjwa ya ngono, Virusi vya UKIMWI pamoja na magonjwa ya
njia ya mkojo (UTI), lakini pia uwepo wa kovu la ukeketaji linalo
kusababisha mimba kinzani na unaweza kusababisha fistula”. alisisitiza
Dkt. Gwajima, na kuongeza kuwa,
“Mtoto anaweza kupata changamoto
wakati wa kujifungua ambapo zinaweza kumsababishia mtindio wa ubongo,
na kupata mateso katika maisha yake yote. aliongeza Waziri Dkt. Gwajima.
Awali
kabla ya kufunga mafunzo hayo, wakichangia mada zilizowasilishwa katika
Kongamano husika, Mangariba hao waliiomba Serikali iwalinde, ili
wasikutwe na madhila kutoka ndani ya Jamii zao.
“Tunapo acha
shughuli za Ukeketaji ni kama tumetangaza vita na wazee wa Mila, lakini
pia Jamii zetu, hivyo Mhe. Waziri, tunaomba sana, tunapo salimisha zana
za Ukeketaji, basi Serikali itungalie namna inavyoweza kutuwezesha ili
tuwe na mitaji na kufanya shughuli mbadala, lakini zaidi sana, tunaomba
tulindwe dhidi ya wanaotutishia, alisisitiza mmoja ya Ngariiba.
Nao
viongozi wa Dini ambao walikuwa Sehemu ya Kongamano hilo, wameitaka
Serikali kubadili mtazamo wa elimu na kutaka elimu husika izidishwe kwa
watoto wa kiume kwani pamoja na kuwachukuwa Wasichana na kuwapeleka
katika makaazi salama kwa wale wanaokimbia vitendo hivyo, kazi bado ipo
kwa wavulana ambao hawana Elimu ya madhila ya ukeketaji kwa mwanamke
“Ndugu
Viongozi na Washiriki wa Kongamano hili, kwa sasa tumewekeza angalau
kwa watoto wa kike, lakini kuna kundi kubwa la wavulana, hawa tumewaweka
nyuma, niiombe Serikali na Wadau, tulitazame kundi hili, alisema”
Sheikh Khalfan Shaban Mtongori.
Kila mwaka, mwezi Februari,
Tanzania huungana na mataifa mengine Duniani kuadhimisha Siku ya
Kimataifa ya Kutokomeza Ukeketaji kwa Wanawake na Watoto.