Nyota wa mieleka Terry Gene Bollea maarufu kama Hulk Hogan afariki dunia

Nyota wa zamani wa mieleka, Terry Gene Bollea maarufu kama Hulk Hogan, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 71 kutokana na kushindwa kwa moyo (cardiac arrest) katika makazi yake Clearwater Beach, Florida, Marekani.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka kwa maofisa wa dharura wa eneo hilo, Hogan alikumbwa na matatizo ya moyo alfajiri ya Julai 24 mwaka huu  na juhudi za kunusuru maisha yake ziligonga mwamba licha ya madaktari na wahudumu wa afya kutumia zaidi ya dakika 30 wakijaribu kumsaidia kwa kumpa huduma ya CPR (Cardiopulmonary Resuscitation).

“Hakukuwa na dalili za tukio la uhalifu. Uchunguzi wa awali unaonesha alifariki kutokana na kushindwa kwa moyo,” amesema msemaji wa idara ya Polisi ya Clearwater.

Hogan, ambaye amekuwa akikumbwa na changamoto za kiafya kwa miaka ya hivi karibuni, aliripotiwa kuwa chini ya uangalizi wa karibu wa kitabibu kutokana na matatizo ya uti wa mgongo na maumivu ya viungo, lakini hakuwa na historia ya dhahiri ya matatizo ya moyo ambayo yangesababisha kifo cha ghafla.

Familia imeeleza kuwa Hogan alilalamika kuhisi maumivu ya kifua na kushindwa kupumua vizuri kabla ya kuanguka ghafla sakafuni. Alipelekwa haraka katika Hospitali ya Morton Plant lakini alitangazwa kuwa amefariki dunia saa 11:17 jioni jana.

Katika taarifa ya familia yake iliyotolewa kupitia wakili wake, ilisomeka: “Tumeumizwa sana na kuondokewa na kipenzi chetu Hogan, lakini tunafarijika kuwa alikuwa amezungukwa na familia na marafiki waliompenda kwa dhati.”


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii