Msanii wa Bongo Fleva
Enock Bella yuko nchini Kenya kwa shughuli za kimuziki kuhakikisha anaongeza
wigo mkubwa katika soko la muziki wake hususan mashabiki wapya ambao wanatakiwa
kuwa nguzo muhimu katika jambo lake.
Sasa akiwa nchini humo,
Enock Bella ameweka wazi kuhusu kile kilichokuwa kinaendelea baina yake na
msanii mwenzake Mbosso kuhusu wao kutokuwa na maelewano mazuri kutokana na
tuhuma za Bella kuwa Mbosso alikataa kumsaidia kimuziki.
Katika mahojiano na
moja ya kituo cha Redio nchini humo weekend iliyopita, Enock Bella amesema kuwa
kuna baadhi ya watu wao wa karibu ambao hawakupenda ukaribu wake na Mbosso hasa
katika changamoto zao, jambo ambalo lilifanya suala hilo kuwa kubwa zaidi hasa
kwa kumfanya mwenzake awe na hasira zaidi kwake.
“Kuna baadhi ya watu
wetu wa karibu ambao walikuwa hawataki kabisa mimi kuwa karibu na Mbosso
kutokana na mahojiano yale niliyayafanya na kumzungumzia. Waliamua kutumia
nafasi hiyo kutuvuruga zaidi wakiamini wananiteketeza zaidi kimuziki lakini
haijawa hivyo” alisema Enock Bella
Pia katika kukazia
zaidi, watu hao anawafahamu vizuri na kama wataendelea kumchonganisha yeye na
Mbosso, itafikia muda atawataja majina hadharani bila kuhofia chochote
Hata hivyo, Enock Bella
alimuomba radhi Mbosso hadharani (kupitia mtandao wa Instagram) na Mbosso
aliridhia bila kinyongo, hali ambayo inatafsiri kuwa wawili hao wamemaliza
tofauti zao