Jeshi la Polisi mkoa wa Rukwa limewakamata wanachama 11 wa Chama cha Demokrasi na Maendeleo (CHADEMA) kati yao wanaume 7 na wanawake 4 wakiwemo viongozi wanne wa chama hicho kwa kufanya mkusanyiko usio halali.
Viongozi hao ni Winfrida Joseph Khenani (Katibu mwenezi wa Baraza la vijana CHADEMA Jimbo la Nkasi Kaskazini), Godfrid Bendera (Katibu wa CHADEMA Jimbo la Nkasi Kaskazini), Evarist Mwanisawa (Katibu Baraza la Wazee CHADEMA Wilaya ya Nkasi) na Scolastica Mwalonde (Mwenyekiti wa CHADEMA kata ya Majengo).
Jeshi la Polisi mkoa wa Rukwa linawataka Mhe. Aida Khenani (Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini) na Albeto John Kaliko 'Galincha' (aliyekuwa diwani wa kata ya Itete) kujisalimisha Polisi wilaya ya Nkasi au ofisi ya mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai mkoa wa Rukwa kwa kupanga mkusanyiko huo usio halali.
Kufuatia kukamatwa kwa wanachama hao wa CHADEMA, kumeibuka watu wanaotuma taarifa za uongo, upotoshaji na za kubuni kwenye mitandao ya kijamii wakiwa na lengo la kuitia hofu jamii ya watanzania au kulichonganisha jeshi la Polisi kwa wananchi.
Hivyo Jeshi la Polisi mkoa wa Rukwa linamtaka mtu mmoja aitwaye Alfred Sotoka kuripoti ofisi ya mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai mkoa wa Rukwa kufuatia kutuma taarifa za uongo kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na tukio hili. Asijifiche kwani atasakwa popote alipo.