Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, imepitisha rasmi majina ya wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi, ikiwemo ubunge na uwakilishi kwaajili ya kwenda kupigiwa kura za maoni na wajumbe watakaochagua mgombea mmoja ambaye atasimama kukiwakilisha chama katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 Oktoba mwaka huu.
Uamuzi huo umetolewa katika kikao maalum kilichofanyika jijini Dodoma, kikiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza na wanahabari mkoani Dodoma mara baada ya kikao hicho, Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), CPA Amos Makalla amesema majina yaliyopitishwa yanatokana na mchakato wa kina wa kuchambua, kupima sifa na uwezo wa wagombea waliowasilisha nia ya kugombea kupitia tiketi ya CCM.
Katika taarifa rasmi iliyotolewa Jumanne Julai 29, 2025 katika Ofisi za Chama hicho Jijijini Dodoma imeelezwa kuwa kuwa katika Jimbo la Ubungo walioteuliwa uteuzi wa awali ni watano akiwemo Prof. Kitila Mkumbo.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kampeni za uchaguzi zitaanza rasmi Agosti 28 na kumalizika tarehe 28 Oktoba 2025.