Maagizo sita (6) yatolewa kwa Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dkt. Moses Kusiluka ametoa maagizo sita (6) kwa Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma yenye lengo la kuongeza ufanisi wa taasisi wanazoziongoza ili kupunguza utegemezi wa ruzuku kutoka serikali kuu. 

Maagizo hayo yaliyotolewa Jumatatu, Julai 28, 2025, ni pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kudhibiti matumizi yasiyo na tija, pamoja na kujenga uwezo wa ndani wa taasisi kwa kuboresha rasilimali watu, teknolojia na miundombinu.

Maagizo mengine ni kuongeza faida kwa taasisi za kibiashara, kuboresha huduma kwa taasisi za huduma, kujiimarisha kwenye matumizi ya TEHAMA, na kila taasisi kutekeleza Dira 2050 kwa nafasi yake.

Maelekezo hayo yalitolewa katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha, Mkoani Pwani wakati wa ufunguzi wa mafunzo elekezi ya siku nne kwa wakuu wa taasisi za umma yalioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kushirikiana na Taasisi ya Uongozi.

Balozi Dk. Kusiluka alisema katika mwaka huu mpya wa fedha angependa kuona taasisi za umma zinaepuka matumizi yasiyo na tija, na kuelekeza fedha zaidi katika maeneo ya vipaumbele vya kitaifa kama vile miundombinu, afya, elimu, na huduma za kijamii.

“Watendaji Wakuu wanalo jukumu la kuhakikisha taasisi zao zinaendeshwa kwa misingi ya ufanisi na uwajibikaji mkubwa,” alisema Katibu Mkuu Kiongozi wakati wa ufunguzi wa mafunzo yaliyowaleta pamoja wakuu wa taasisi za umma 114.

Balozi Dkt. Kusiluka aliongeza kuwa ili taasisi za umma ziongeze ufanisi, zinapaswa kujenga uwezo wa ndani wa taasisi kwa kuboresha rasilimali watu, teknolojia na miundombinu.

Aidha, alizitaka taasisi za umma, kila moja kwa nafasi yake, kuhakikisha zinashiriki katika kufanikisha Dira 2050.

Dira hii inalenga kuiwezesha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati wa juu, yenye viwanda, mifumo ya kiutawala yenye uwazi, na ustawi kwa wananchi wote.

“Tunatarajia pato la Taifa kufikia $1 trilioni ifikapo 2050, huku pato la mtu mmoja mmoja likifia $7,000, hii sio kazi ndogo lakini tuna kila sababu ya kufikia lengo,” alisema Dkt. Kusiluka.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii