Aliyekuwa mkuu wa mkoa Arusha, Paul Makonda na wengine sita kuwania ubunge CCM Jimbo la Arusha Mjini.

KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, imepitisha rasmi jina la aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda na wagombea wengine sita kuwania ubunge wa CCM katika Jimbo la Arusha Mjini. 

Miongoni mwa majina ambayo hayakupitishwa ni la Mrisho Gambo, aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo.

Majina ya waliopitishwa ni Ally Said Babu, Hussein Omarhajji Gonga, Aminatha Salash Toure, Mustapha Said Nassor, Makonda, Lwembo Mkwavi Mghweno na Jasper Kisumbua.

Taarifa rasmi kuhusu uteuzi huo imetolewa leo Jumanne, Julai 29, 2025, katika Ofisi za CCM jijini Dodoma na Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo, CPA Amos Makalla.

Katika taarifa hiyo, Makalla ameeleza kuwa mchakato wa awali wa uteuzi katika Jimbo la Arusha Mjini ulihusisha wagombea saba, ambapo baada ya tathmini ya sifa na uwezo, Paul Makonda ameibuka kidedea.

Kwa mujibu wa Makalla, uteuzi huo umezingatia vigezo vya uongozi, uwezo wa kisiasa, maadili, na mapokezi kutoka kwa wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla. Alisisitiza kuwa CCM inaendelea kuimarisha misingi ya kidemokrasia kwa kuhakikisha inatoa wagombea wenye uwezo wa kweli kuwatumikia wananchi.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii