Uzinduzi wa Dira ya taifa ya 2050 yaja na maagizo sita ya utekelezaji

Rais  Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa Watanzania wote kujielekeza katika kutekeleza kwa vitendo Dira ya Taifa 2050 badala ya kuishia kwenye maneno. 

Amesema tabia hiyo haimhusu mtu mmoja au kundi fulani, bali ni changamoto ya kitaifa inayohitaji kushughulikiwa kwa pamoja. 

Rais amesisitiza kuwa ili dira mpya iwe na mafanikio, ni lazima serikali, sekta binafsi, na wananchi kwa ujumla washirikiane kwa vitendo, kila mmoja akitimiza wajibu wake.

Hata hivyo ametoa maelekezo sita kwa taasisi za umma na sekta binafsi kubadili mtazamo na namna ya kupima mafanikio ili kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.

Kwa kuwataka watu kubadili mitazamo na kuacha kufanya kazi kwa mazoea, ametaka kila wizara kupitia upya sera zake na kuhakikisha zinaendana na mwelekeo wa dira hiyo mpya ya taifa. 

Aidha, ameagiza kuboreshwa kwa mfumo wa ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo ili kuhakikisha uwajibikaji na tija.

Kwa upande mwingine, Rais amezitaka sekta binafsi kujipanga vema kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa malengo na shabaha za dira hiyo huku akisisitiza umuhimu wa kulinda haki na utamaduni wa Mtanzania kama sehemu ya mwelekeo wa maendeleo ya taifa.



Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii