Jeshi la Polisi nchini Kenya limewekwa kwenye mzingo wa shinikizo kutoka kwa familia, mashirika ya haki za binadamu na umma, baada ya kumkamata mwanaharakati maarufu Boniface Mwangi kwa tuhuma za ugaidi na uchomaji mali kuhusiana na maandamano ya kitaifa ya tarehe 25 Juni 2025.
Kukamatwa kwa Mwangi nyumbani kwake Lukenya na upekuzi uliofuata ofisini kwake, ambako maafisa walichukua vifaa kadhaa ikiwemo laptop, simu, mihuri na daftari la hundi, kumewasha moto wa mjadala kuhusu matumizi ya nguvu dhidi ya wanaharakati.
Hali hiyo imezidi kutia wasiwasi baada ya familia yake kushindwa kuthibitisha kama anazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Pangani, licha ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kudai hivyo. Kauli za utata kutoka kwa maafisa wa usalama zimezusha hofu juu ya usalama na haki zake za kisheria, huku wito ukitolewa kwa serikali kueleza wazi mahali alipo na kuhakikisha analindwa kisheria.
Kwa mujibu wa wakili wake, hatua hiyo ni sehemu ya mikakati ya kuwakandamiza viongozi wa kiraia wanaotumia sauti zao kuikosoa serikali. Mashirika ya haki za binadamu yameonya kuwa matumizi ya sheria za ugaidi dhidi ya wanaharakati ni hatari kwa demokrasia na huandaa mazingira ya ukandamizaji wa uhuru wa kujieleza.
Mwangi anatarajiwa kufikishwa mahakamani leo, Jumatatu, ambapo atasomewa mashtaka ya kufadhili ugaidi na kumiliki risasi kinyume cha sheria tuhuma ambazo watetezi wa haki za binadamu wanasema ni njama ya kuwatisha wapigania haki.